News
WATENDAJI SEKTA YA MAJI WATAKIWA KUACHA ALAMA KWA KULETA MATOKEO
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) leo imesaini mkataba wa utendaji kati yake na Wizara ya Maji.
Mkataba huo umesainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DUWASA, Bw. Fadhili Chibago pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph mbele ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri leo jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka Wenyeviti wa Bodi kuhakikisha wanasimamia Mamlaka za Maji ili kuleta matokeo chanya
Waziri Aweso amesema mikataba iliyotiwa saini ni ahadi ya uwajibikaji na ufanisi kwa watendaji katika kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha malengo na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameongeza kuwa uongozi sio cheo , uongozi ni alama hivyo Watendaji wa Sekta ya Maji wametakiwa kuacha alama katika utendaji wao kwa kuzingatia matokeo, uwajibikaji na ubora wa huduma za maji kwa kila mwananchi.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema sekta ya maji inaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa vipimo vya utendaji kazi vitatumika kama kigezo cha kupima uwezo na ufanisi wa watendaji kuendelea kubaki katika nafasi zao.
Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Wenyeviti wa Bodi za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA, Bw. Fadhili Chibago amesema wamepokea maelekezo yote na wanaahidi kwenda kuyatendea kazi kama alivyoelekeza.