News

Posted On: Jun, 13 2022

WANAWAKE NDACHI, MATULI KUTULIWA NDOO KICHWANI

News Images

WANANCHI wa eneo la Ndachi na Matulia wanatarajia kupata Majisafi na Salama mwishoni mwa mwezi huu ikiwa ni moja ya lengo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kutatua changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali ya pembezoni mwa jiji.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mhandisi wa Mradi wa Ndachi Mnadani, Mhandisi David Kasanja.

Amesema Mradi huo unaotekelezwa na WaterAids kwa kushirikiana na DUWASA ambao unagharimu Shilingi Milioni 235 na utahudumia Kaya zaidi 2000 ambazo zinapatikana eneo la Ndachi Mnadani.

“Mradi huu unahusisha ujenzi wa tanki kubwa la lita 135,000, ukarabati wa kisima, nyumba ya kuhifadhia pampu, vituo viwili vya kuchotea maji na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa umbali wa kilomita 5. Mradi huu ulianza Februari 18 na tunatarajia kuukamilisha mwishoni mwa mwezil Julai mwaka huu”. Alisema Mhandisi Kasanja.

Naye Afisa Maenedeleo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Hidaya Mizega amewataka wananchi kushirikiana katika kuusimamia na kuulinda Mradi mpaka utakapokamilika.

“Tusiwaruhusu wenye nia ovu, wenye nia mbaya wakaharibu miundo mbinu ya Mradi wa Maji, hata kama ni mtoto wako au ndugu yako, wakikamatwa atashughulikiwa kwa sheria za nchi” alisema Hidaya.

Kwa upande wa wananchi, Elizabeth Shija anasema wao wameupokea mradi huo kwa moyo mmoja kwa sababu maji ilikuwa ni changamoto kubwa sana hivyo wanashukuru kwa mradi kuwafikia kwani watu wengi wameshindwa kwenda kujenga kutokana na changamoto hiyo ya maji.

Mohamed Omary amesema wanashukuru kwa sababu Mradi utawatua kina mama ndoo kichwani, walikuwa wananchota maji maeneo ya mbali na kwa gharama kubwa.