TANGAZO

Posted On: Nov 27, 2020


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kwa kushirikiana na Benki ya Equity wameanzisha utaratibu wa kuwezesha mikopo kwa wateja wapya wanaohitaji kukopeshwa fedha kwa ajili ya maunganisho ya majisafi na majitaka. Huduma hii ya uwezeshwaji kwa njia ya mkopo imeanzishwa kufuatia maombi ya wananchi ya muda mrefu ambayo yameonyesha kuwepo na uhitaji wa huduma hii.

Utaratibu ni kwamba kwa wateja wanaohitaji huduma hii wanafika ofisi ya maunganisho mapya ya majisafi na majitaka DUWASA ambapo mafundi wa DUWASA watafika eneo la mteja na kupata vipimo halisi vya eneo la mteja na baada ya hapo DUWASA itaandaa fomu yenye gharama hizo. Mteja atawasilisha fomu yenye gharama zake za maunganisho ya majisafi au majitaka Benki ya Equity kwa ajili ya maombi ya kupatiwa mkopo husika.

Benki ya Equity itampatia mwananchi mhitaji mkopo husika kwa riba yenye unafuu mkubwa kulingana na chanzo cha ulipaji wa mkopo. Fedha hizo za mkopo zitalipwa kwenye akaunti ya DUWASA ambapo mteja atarejea DUWASA kwa ajili ya kuunganishiwa huduma ya majisafi au majitaka. Mteja ataunganishiwa huduma na kutakiwa kulipa deni lake la mkopo kwa Benki ya Equity huku akiendelea kunufaika na huduma ya DUWASA kwa kulipa bili yake ya kila mwezi ya majisafi au majitaka.

Imetolewa na;

MKUU WA KITENGO CHA MAWASILIANO

Sebastian V. Warioba

DUWASA

26 NOVEMBA 2020