News

Posted On: Aug, 19 2026

WANANCHI 880 CHAMWINO WALIPWA FIDIA KUPISHA HIFADHI YA CHANZO CHA MAJI

News Images

Serikali kupitia Wizara ya Maji imeanza rasmi kuwalipa fidia wananchi 880 wa vitongoji vya Mpera na Sokoine wilayani Chamwino, mkoani Dodoma, kiasi cha shilingi bilioni 4.928, ili kupisha na kulinda eneo la hifadhi ya chanzo cha maji cha Bonde la Chamwino.

Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mingi kati ya wananchi na Serikali, huku ikilenga kuhakikisha chanzo hicho kinahifadhiwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji ya uhakika na endelevu kwa wakazi wa Dodoma.

Akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Chamwino wakati wa hafla ya kuwasilisha malipo hayo, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, alisema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kutambua umuhimu wa chanzo hicho katika kukidhi mahitaji ya maji yanayoongezeka katika Jiji la Dodoma.

Alisema tangu Serikali ilipohamia Dodoma mwaka 2017, mahitaji ya maji yameongezeka kwa kasi kutoka lita milioni 45 kwa siku hadi lita milioni 159 kwa siku, wakati uzalishaji wa sasa ukiwa takribani lita milioni 88 kwa siku.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, hali hiyo inaifanya hifadhi ya vyanzo vya maji kuwa jambo la msingi katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika, hususan wakati mahitaji yakiendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.

Kundo alisema eneo la Bonde la Chamwino lilitengwa tangu kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, lakini mchakato wa kuwalipa wananchi walioathiriwa umefanikishwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema eneo hilo lilitengwa awali likiwa na ukubwa wa takribani ekari 740, ambapo kati ya mwaka 1970 na 1980 Serikali ilichimba mabwawa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima na wafugaji.

Alisema baada ya Dodoma kutangazwa kuwa makao makuu ya nchi mwaka 1973, mahitaji ya maji yaliongezeka na eneo la hifadhi likapanuliwa hadi kufikia takribani ekari 2,100, hatua iliyohusisha maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na wananchi na baadaye kusababisha migogoro ya ardhi.

Mhandisi Waziri alisema Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maji iliunda timu ya wataalamu iliyofanya tathmini na kupendekeza Serikali izingatie eneo la awali la ekari 740 katika hatua za kulinda chanzo hicho.

Alisema mchakato wa uthamini wa ardhi na mali ulianza rasmi Agosti 2024, ukihusisha wananchi kupitia mikutano ya kutoa elimu pamoja na uwekaji wa mipaka ya eneo hilo.

Aidha, alifafanua kuwa fidia hiyo inalipwa kwa wananchi waliothibitika kuathirika na eneo la hifadhi, huku taasisi za Serikali kama shule na miradi mingine ya umma zikishughulikiwa kupitia utaratibu mwingine wa Serikali.