News
UJENZI WA MABWAWA YA KUTIBU MAJITAKA DODOMA, WAFIKIA ASILIMIA 17
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Maji, inaendelea na ujenzi wa Mradi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka unaotarajiwa kuhudumia Mji wa Serikali (Magufuli City). Hadi sasa mradi umefikia asilimia 17 ya utekelezaji.
Mradi huo, unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kupitia kwa Mshauri NORPLAN (T) LTD, ulianza rasimi tarehe 1 Juni 2026, ukitekelezwa na Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd. (BCEG).
Mradi huo unajengwa katika Kata ya Buigiri, Wilaya ya Chamwino, kwa gharama ya Shilingi bilioni 31.9, na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ifikapo Juni 2027.
Kwa sasa, Mkandarasi anaendelea na kazi mbalimbali za ujenzi zikiwemo uchimbaji wa Mabwawa na mitaro, ulazaji wa mabomba, pamoja na ujenzi wa majengo ya ofisi, maabara, nyumba ya watumishi na kibanda cha mlinzi.
Mradi huu unatarajiwa kuboresha huduma za usafi wa mazingira na uondoshaji wa Majitaka katika Mji wa Serikali, hatua itakayochangia kupunguza uchafuzi wa mazingira, sanjari na maono ya Serikali ya kujenga Miji ya kisasa yenye miundombinu bora ya Majisafi na Usafi wa Mazingira.