News

Posted On: Mar, 01 2023

SERIKALI YAWEKEZA BIL. 9.14 KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI DODOMA

News Images

Serikali kupitia Wizara ya Maji na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 9.14 katika kutekeleza miradi kama hatua za muda mfupi kukabiliana na ongezeko kubwa la mahitaji ya maji jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa leo Februari 28, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph wakati wa Mkutano na Waandishi wa habari katika kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili Jijini Dodoma.

Amesema kwa sasa DUWASA inazalisha nusu ya mahitaji ya maji ambapo mahitaji ya maji ni lita milioni 133 kwa siku na unazalishaji ni lita milioni 67.8 hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 66.7 kwa siku. Upungufu huu unaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi na kijamii katika Jiji la Dodoma.

“Tayari visima vitano vimeshachimbwa eneo la Nzuguni vyenye uwezo wa kuzalisha lita million 7.6 kwa siku. Mradi huu utahusisha pia ujenzi wa miundombinu ili kuyafikisha maji hayo haraka kwa wakazi wapatao 37,000 wa Nzuguni, Ilazo Swaswa na Kisasa na kuboresha hali ya upatikanaji wa maji Jijini Dodoma. Mradi huu utagharimu takribani bilioni 5.8” Amesema Mhandisi Joseph.

Aidha Mhandisi Joseph amesema Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 23.8 kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji kwa maeneo ya pembezoni kama mpango wa muda mfupi ili kupunguza adha ya upatikanaji wa maji. Fedha hizi ni kwa ajili ya kuchimba visima maeneo ya Bihawana na Zuzu.

“Mpango wa dharura wa kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma ni kutoa maji Bwawa la Mtera na kuyaleta Dodoma ili kutosheleza mahitaji ya maji kwa kwa sasa na baadae. Mradi huu umefikia hatua ya usanifu ili uanze kutekelezwa. Mradi utaongeza kiasi cha maji lita milioni 130 kwa siku na utagharimu shilingi bilioni 326”. Amesema Mhandisi Joseph

Kwa Upande wa majitaka Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni bilioni 161 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya majitaka katika jiji la Dodoma ambapo Kata 14 ambazo hazijafikiwa kabisa na huduma zitaanza kuhudumiwa.

Aidha kiasi cha shilingi bilioni 4.9 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa mtandao wa majitaka eneo la Area C na D ili kuondoa adha ya harufu mbaya na kuziba kwa mtadao huo mara kwa mara.