News
MWENYEKITI BODI YA DUWASA AZIPA MAAGIZO MAMLAKA ZA KIBAIGWA NA MPWAPWA

Na Bonna Tibaijuka, DUWASA
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA), Profesa Faustine Bee amezitaka Mamlaka za maji za miji ya Kibaigwa na Mpwapwa kuhakiklisha zinadhibiti upotevu wa maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kwa Wananchi pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Profesa Bee amesema hayo yakifanyika kikamilifu na kwa haraka yatasaidia kuwezesha Mamlaka hizo kujiendesha zenyewe bila usimamizi wa DUWASA kama ilivyo sasa.
Kauli hiyo imetolewa Jumamosi ya tarehe 16 Oktoba 2021 wakati Bodi hiyo ilipotembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpwapwa (MPWUWSA) pamoja na Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Kibaigwa (KIBAWASA) kisha kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ya uchimbaji wa visima inayoendelea.
“Tunahitaji kufanya uwekezaji zaidi, ongezeni ubunifu wa namna ya kupambana na upotevu wa maji, kukusanya mapato na kuandika maandiko ya miradi inayohitaji ufadhili,” alisema Profesa Bee.
Alisema sehemu kubwa inayochangia upotevu wa maji ni uchakavu wa miundombinu na wizi wa maji hivyo kunahitajika kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kufikisha huduma bora na ya haraka kwa Wananchi.
''Tutoke kwenye asilimia 69 tulipo sasa na tufike asilimia 100 katika kuwafikishia huduma ya maji, kila mwananchi anufaike, lengo letu ni kumtua mama ndoo kichwani kama haya yatafanyika ipasavyo sioni sababu ya nyie kuwa chini ya usimamizi wa DUWASA, mnatakiwa kuwa Mamlaka kamili inayojitegemea,'' alisema Prof. Bee
Aidha, amesema kuwa lengo la DUWASA ni kuwa Mamlaka bora nchini na kwa sasa DUWASA Imeanza kuboresha uwekezaji katika usafi wa mazingira, ambapo amewataka MPWUWSA na KIBAWASA kuanza kufikiria namna ya kujenga mtandao wa majitaka pamoja na kutafuta maeneo kwa ajili ya kujenga mabwawa ya kutibu na kuhifadhi majitaka.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira MjiniMpwapwa (MPWUWSA), Mhandisi Peter Kabelwa, alisema baada ya miaka mitatu Mamlaka hiyo itakuwa inajitegemea baada ya kufanyia kazi masuala muhimu, ikiwemo la upanuzi wa mtandao wa majisafi na kuongeza uzalishaji kwa kuchimba visima vikubwa vya maji.
Pia, alibainisha changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na uchakavu wa miundombinu katika vyanzo vya maji vya Mayawile na Kwamdyanga ambapo alisema vipo kwenye hatari ya kuchukuliwa na maji ya mvua hasa eneo la Kikombo.
Katika kudhibiti uharibifu kwenye chanzo hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, ameitaka MPWUWSA kufanyia kazi kwa haraka suala hilo kabla mvua hazijaanza kunyesha na kuepusha athari zaidi kwa chanzo hicho kutoweka.
“Kuna madeni makubwa ambayo Mamlaka inazidaitaasisi za Serikali, mtandao mdogo wa maji usioendana na ukuwaji wa maeneo ya huduma na gharama kubwa za uendeshaji,” alisema Mhandisi Kabelwa.
MPWUWSA ina mtandao wa maji wenye urefu wa kilomita 58.1, matanki ya kuhifadhia maji manne yenye ujazo wa lita milioni 2 huku ikihudumia kata tatu ambazo ni Mpwapwa Mjini, Vingh'awe na Mazae ikiwa na jumla ya wateja 3466.
Pia, Bodi ya Wakurugenzi ya DUWASA imeipongez Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mji wa Kibaigwa (KIBAWASA) kwa juhudi za kuboresha huduma na kuongeza mapato kutoka wastani wa shilingi milioni 37 kwa mwezi hadi shilingi milioni 68 kwa mwezi. Kupitia wataalam wake, Bodi imeitaka KIBAWASA kuongeza ubunifu katika ukusanyaji wa mapato, kupata wafadhili na kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha inafikisha huduma ya maji kwa urahisi kwa wakazi wa Kibaigwa.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dk. Fatuma Mganga ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ameitaka KIBAWASA kuangalia kama kuna eneo lolote lakupunguza gharama za uendeshaji na kujipanga kwa ujio wa mitambo ya uchimbaji wa visima na mabwawa ili kuongeza uzalishaji wa maji kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji KIBAWASA, Mhandisi Oscar Bakari amesema kupitia kiasi cha fedha Shilingi milioni 950 walichopatiwa kutoka Wizara ya Maji wameweza kufunga pampuna miundombinu mingine katika visima vilivyokuwa havina miundombuni, kutanua mtandao wa maji katika mji wa KIBAIGWA kwa urefu wa kilomita 7.8 na NDURUGUMI kwa urefu wa kilomita 23 na piampango uliopo ni kuchimba visima vingine vikubwa vinne tofauti na vilivyopo sasa.
Mbali na hilo, Mhandisi Bakari amesema changamoto wanayokumbana nayo ni uvamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji, watu kujenga juu ya miundombinu ya maji na wengine kulima pembezoni ya visima vya maji, hivyo kuhatarisha vyanzo kwa kuweza kusababisha kukauka na kuchafuliwa.
Pia, changamoto nyingine kubwa ni kukatika katika kwa umeme na unapokuwepo kuwa na nguvu ndogo hivyo kushindwa kuendesha mitambo kwa saa 24 na kupelekea muda wa mchana kutumia zaidi jenereta hali inayosababisha gharama kubwa za uendeshaji.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi DUWASA, Profesa Bee ameitaka mamlaka hiyo kufanya mazungumzo na Shirika la Umeme TANESCO pamoja na Idara ya Ardhi ili kuwaondoa wakazi wote waliojenga na wanaofanya shughuli karibu na vyanzo vya maji na kulipwa fidia kwa wale watakaostahili.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kibaigwa ina mtandao wa maji safi wenye jumla ya kilomita 63.88 ina jumla ya visima sita, vitano vikiwa eneo la Mbuyuni na kisima kimoja kipo eneo la Ndurugumi, ambapo kati ya visima hivyo vinvyofanya kazi ni visima vitano.