News
MRADI WA MAJI WA NZUGUNI KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI SITA

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA), imeanza kutekeleza mradi wa maji katika Kata ya Nzuguni utakaonufaisha wakazi 37,929 na unatarajiwa kukamilika Agosti 2023.
Mradi huo ni wa ujenzi wa mantanki mawili, ulazaji wa mabomba na uchimbaji wa visima vitano vitakavyohudumia maeneo ya Nzuguni, Swaswa, Ilazo na Kisasa, hadi kukamkilika kwake utagharimu kiasi cha sh. Bilioni 4.8.
Hayo yamebainishwa jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipotembelea mradi huo.
“Chimbuko la mradi huu ni uhaba wa maji takribani asilimia 50 katika jiji la Dodoma, DUWASA na Wizara ya Majiwameendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji wakati serikali ikiendelea kutatua changamoto iliyosababishwa na ongezeko kubwa la wat una shughuli za kiuchumi,”alisema Mha. Aron.
“DUWASA inamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maji kwa kutekeleza mradi huu katika jiji la Dodoma. Mradi huu utawahakikishia wananchi upatikanaji wa maji na kuondokana na migao iliyopo sasa,”amesema Mhandisi Joseph.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma(PIC), Jerry Silaa ameipongeza DUWASA kwa kazi nzuri ya kusambaza maji katika jiji la Dodoma kupitia miradi mbalimbali.
Amesema mradi huo kwa kiasi kikubwa utapunguza mgao wa maji katika maeneo mengi ya jiji na utarudisha fedha ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
“Tunatoa wito kwa mkandarasi afanye kazi haraka ili mradi huu ukamilike kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.”alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya, Charles Mamba ameipongeza DUWASA kwa jinsi wanavyotekeleza miradi ya maji ili kupunguza migao pia ameipongeza kamati kwa kutembelea mradi ili kujionea namna unavyotekelezwa.
Naye Judith Odunga, Rais wa Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania, ameshukuru serikali kwa kumuamini na kumpa kandarasi kutekeleza mradi huu huku akiiomba iharakishe upatikanaji wa fedha ili aweze kukamilisha mradi huu kwa wakati.
Diwani wa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega amesema kwamba kilio kikubwa cha Wananchi wa eneo la Nzuguni ni maji hivyo kuitaka DUWASA kukamilisha mradi kwa wakati.