News

Posted On: Mar, 03 2023

MKURUGENZI MKUU WA EWURA AIPONGEZA DUWASA KWA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI DODOMA

News Images

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile, jana tarehe. 2/3/2023 amefanya ziara ya kikazi katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ili kujionea shughuli za utendaji na utekelezaji wa miradi ya maji zinazofanywa na Mamlaka.

Dkt. Andilile ameupongeza Uongozi wa DUWASA kwa juhudi wanazofanya katika kupambana na changamoto ya uhaba wa maji katika jiji la Dodoma, kuongeza kiasi cha maji na kuongeza mtandao wa majisafi na majitaka.

Aidha Dkt. Andilile ameitaka Menejimenti ya DUWASA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya maji ili kuwapunguzia gharama za huduma, kupunguza upotevu wa maji na kulinda miundombinu ili huduma iwe endelevu.

“Hapa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi lazima huduma ya maji iwe bora, DUWASA mnawajibika kutoa huduma bora ya majisafi na majitaka kwa Wananchi. EWURA tuna wajibu kuhakikisha huduma zina ubora, zinapatikana na endelevu, kwani wote tupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi” alisema Dkt. Andilile.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mha. Aron Joseph, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa EWURA kwa kutembelea DUWASA na pia kwa ushirikiano ambao EWURA inaotoa katika kuhakikisha huduma inakua bora.

Mhandisi Aron amesema DUWASA itafanyia kazi maelekezo yote yanayotolewa na EWURA katika kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani.