News
KATIBU MKUU WA CCM AKAGUA MRADI WA MAJI NZUGUNI

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Daniel Chongolo ameipongeza Serikali katika kutatua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma.
Chongolo ameyasema hayo wakati alipokwenda kukagua mradi wa maji Nzuguni unaogharimu shilingi bilioni 4.8 ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake mkoani humu.
Alisema Serikali imefanya kazi kubwa katika kutatua changamoto ya maji kwa kutekeleza miradi ya maji.
"Kazi kubwa inayofanywa katika kutekeleza miradi ya maji kunatafsiri kuwa mnaelekea kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi na kuimarisha uhai wa wananchi, kwa hayo ni muhimu kwa kweli niipongeze sana serikali." Alisema Chongolo
Naye Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde aliomba serikali kuharakisha ulipaji fidia kwa wananchi ambao wameridhia kupitisha mradi wa maji Nzuguni.
Pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia uchimbaji wa visima pembezoni ikiwemo mradi wa Nzuguni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema mradi umefika asilimia 74 na unaendelea na ujenzi wa vibanda vya kuendeshea visima, ujenzi wa ofisi ya kuendeshea miradi, kuagiza pampu za kusukumia maji na ujenzi wa misingi ya matenki ya lita milioni 3.5.
Amesema zoezi la uthamini na malipo yafanyike katika ekari 2.7 ya viwanja 58 vilivyoguswa na miundombinu ya maji tayari uthamini umefanyika na watu 24 wanaomiliki viwanja 25 wametambuliwa.
Aidha ofisi ya jiji la Dodoma inaendelea na awamu ya pili ya utambuzi wa wamiliki wa viwanja 33 ambavyo vimebaki, pia alisema wananchi wote ambao wapo katika eneo la Nzuguni A waendelee na shughuli zao za kuendeleza viwanja wanavyomiliki isipokuwa viwanja 58 tu.
Mhandisi Joseph amesema utekelezaji wa mradi huo katika Kata ya Nzuguni utanufaisha wakazi wapatao 75,968 wa eneo la Nzuguni na maeneo ya jirani ya Ilazo, Swaswa na Nyumba 300 na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.