News
DUWASA YADHAMIRIA KILA TONE LA MAJI LINAMFIKIA MWANANCHI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kushirikiana na Shirika la VEi kutoka Uholanzi, imeanza rasmi mkakati mpya wa kukabiliana na changamoto ya upotevu wa maji kwa kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo maalum ya kiufundi na kiutendaji.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yameanza Septemba 8, 2026 na yamehusisha Wajumbe wa Kamati ya Kudhibiti Upotevu wa Maji pamoja na Timu ya Ufundi ya Kudhibiti Upotevu wa Maji kutoka DUWASA, ikiwa ni hatua ya kimkakati ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ya maji safi kwa wakazi wa Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa DUWASA, Mhandisi Bernard Rugayi, amewataka washiriki kuyachukulia mafunzo hayo kwa uzito mkubwa kwa kuwa ndiyo msingi mkuu wa vita dhidi ya upotevu wa maji ndani ya Mamlaka.
"Mafunzo haya ni muhimu sana na yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa hali ya juu kwani ndio mwanzo rasmi na msingi wa kupambana na upotevu wa maji. Kuimarisha uwezo wa timu zetu ndiko kutakakotuwezesha kulinda rasilimali hii na kuhakikisha maji yanawafikia wananchi kama ilivyokusudiwa," alisema Mhandisi Rugayi.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Bw. Bernard Mbatia, Mtaalamu na Mkufunzi wa masuala ya Upotevu wa Maji kutoka nchini Kenya na yamelenga kutoa mbinu za kisasa za kubaini, kuzuia, na kupunguza upotevu wa maji unaotokana na miundombinu chakavu au changamoto za kiufundi.