News

Posted On: Jul, 08 2020

DUWASA YABORESHA HUDUMA ZA MAJISAFI NA UONDOSHAJI MAJITAKA JIJINI DODOMA

News Images

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kwa kushirikiana na Serikali pamoja na Washirika wa Maendeleo katika Sekta ya maji imepanga kuendelea kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dodoma ili kuepuka kero na adha za upungufu wa maji kwa wakazi wa Jiji.

Akitoa taarifa ya hali ya maji katika Jiji la Dodoma kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi David T Pallangyo alisema kuwa DUWASA ina mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dodoma.

“Mipango ya uboreshaji ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na baadhi ya mipango inatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2020/2021. Umuhimu wa kutekeleza mipango hii unasukumwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano (5) kuhamia Makao Makuu ya Nchi – Dodoma ambapo uhamiaji wa Serikali Dodoma umesababisha ongezeko la uhitaji wa huduma nyeti ya maji ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi siku hadi siku”, Mhandisi Pallangyo alibainisha.

Alisema kuwa mipango ya muda mfupi inaendelea kutekelezwa na DUWASA na mingine inatarajiwa kuanza katika kipindi kifupi kijacho. Alisema miradi inayoendelea ni ile ya kusambaza maji maeneo yasiyo na hudumakwa sasa ambayo ni pamoja na Mlimwa Hill, Michese, Mkalama, Mkonze na Ntyuka yote hii kwa kutumia uwezo wake wa ndani.

Katika mwaka wa fedha 2019/2020, DUWASA ilitenga Shs. 2.02Bn/= kwa ajili ya kusogeza huduma ya maji kwenye maeneo hayo. Aidha, aliendelea kusema kuwa, katika mwaka wa fedha 2020/2021, DUWASA imetenga jumla ya shilingi 2.2Bil/- na imepanga kukopa Shs. 1.5bn/= kupitia mfuko wa Investiment Financing Facilities (IFF) unaofadhiliwa na KfW kwa kushirikiana na Wizara ya Maji ili kuwezesha usambazaji maji katika maeneo mbalimbali Jijini.

Vilevile Mkurugenzi alisema kuwa, DUWASA kwa kutumia uwezo wake wa ndani imetekeleza mradi wa majitaka eneo la Kigamboni umbali wa mita 750 kwa kulaza mabomba ya kipenyo cha milimita miambili hamsini 250(10”) ambapo imegharimu jumla ya shilingi milioni 57. Wateja zaidi ya 33 ambao wapo karibu na Mtandao huo uliojengwa watanufaika.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, DUWASA imetenga jumla ya shilingi 546mil/- kwa ajili ya kutekeleza miradi ya majitaka kwenye maeneo ya Chamwino (Bonanza), Swaswa, Bahiroad (mtaa wa Kitenge) Chang’ombe, Area A na Kinyambwa.