News

Posted On: Jun, 04 2023

BODI MPYA DUWASA YAZINDULIWA

News Images

BODI mpya ya tisa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), imezinduliwa jana Alhamisi Juni 1, 2023 huku wakiagizwa kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 28 hadi kufikia chini ya asilimia 20.

Agizo hilo, limetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi mara baada ya kuzindua bodi hiyo na mradi wa Majisafi Ntyuka Chimalaa wenye thamani ya Sh471.8 milioni.

Mhandisi Nahundi ameiagiza bodi hiyo kushirikiana na watumishi kuweka mikakati ya kuendelea kuongeza makusanyo ili mamlaka iweze kuboresha utoaji wa huduma huku akiipongeza iliyopita kwakuongeza makusanyo kutoka Sh1.7 bilioni hadi Sh2.2 bilioni kwa mwezi.

Naibu waziri huyo amewata kuendelea kuwahudumia ipasavyo wakazi wa Dodoma huku ikitekeleza miradi ya muda mfupi ya kupunguza changamoto ya ukosefu wa maji wakati Serikali ikitekeleza miradi mikubwa.

Pia, ameiambia bodi hiyo kushirikiana na Menejimenti ya DUWASA kuendelee kusimamia ipasavyo miradi yote ya maji pamoja na kuhakikisha uwepo wa thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali, akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa maji, Naibu Waziri Mahundi ameeleza dhamira ya Rais kumtua mama ndoo kichwani inaendeea kutekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameshauri Dodoma kupewa mpango mkakati wa kipekee wa kutatua changamoto ya maji ili kuendana na uwepo wa makao makuu ya nchi.

Amesema Mkoa wa Dodoma kuna taasisi nyingi ambazo wanafanya nazo kazi huku akiitaja DUWASA kama Mamlaka inayofanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo unanufaisha wakazi wapatao 4,441 ambapo kati ya hao 1,931 wanaishi katika maeneo ya Ntyuka mtaa wa Chimalaa katika awamu ya kwanza, na awamu ya pili itanufaisha wakazi wapatao 2,510 katika mtaa wa Nyerere.

Mwenyekiti wa Bodi aliyemaliza muda wake, Profesa Faustine Bee amesema katika kipindi cha uongozi wao wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongeza urefu wa mtandao wa mabomba ya kukusanya majitaka.

Naye, Mwenyekiti mpya wa bodi, Balozi Job Masima amemshukuru Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa imani aliyomuonesha yeye na wajumbe wengine wa bodi na kuamua kumteua huku akieleza watatekeleza kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kuenzi yaliyoachwa na viongozi waliopita.