News

Posted On: Jun, 12 2026

​WANANCHI BUIGIRI WAPOKEA KWA FURAHA MRADI WA UONDOSHAJI NA KUTIBU MAJITAKA MAGUFULI CITY

News Images

Wananchi wa Kijiji cha Buigiri, Kitongoji cha Chang’ombe Wilayani Chamwino, wameupokea kwa furaha Mradi wa Uondoshaji na Kutibu Majitaka wa Magufuli City unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Juni 15, 2026 chini ya Mkandarasi BCEG kutoka China na Mshauri wa Mradi NOPLAN LIMITED.

Akizungumza katika Kikao cha kutambulisha mradi huo kilichowakutanisha Wananchi na Viongozi wa maeneo husika, Mwakilishi wa DUWASA Mhandisi Daniel Mgunda amewaeleza wananchi umuhimu wa mradi huo pamoja na manufaa yatakayopatikana wakati wa utekelezaji wa mradi na baada ya kukamilika kwake.

Wananchi wameonyesha utayari wa kushirikiana na DUWASA, Mkandarasi na Wasimamizi wa mradi ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa ufanisi.

Kwa upande wao Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wameahidi kutoa ushirikiano wa karibu na kushiriki katika utatuzi wa changamoto zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.

Aidha, kikao hicho kimekubaliana kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Wananchi na Viongozi wa maeneo yanayopitiwa na mradi ili kusaidia uratibu wa shughuli za mradi na kushughulikia changamoto zitakazojitokeza wakati wa utekelezwaji wa mradi huo.

Viongozi wa maeneo husika wakiwemo Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Mabalozi na Wajumbe wameipongeza Serikali kwa kuleta mradi huo na kuahidi kushirikiana kikamilifu katika kuhakikisha unatekelezwa na kukamilika kwa wakati na ufanisi.