News
CCM DODOMA YAIPONGEZA DUWASA KWA MAPINDUZI YA MAJI, YALENGA ASILIMIA 100 IFIKAPO 2030
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kimeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kasi kubwa na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji, hatua inayotajwa kuwatoa wananchi wengi katika kero ya muda mrefu ya uhaba wa maji.
Pongezi hizo zimetolewa Juni 6, 2026 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Ndugu Jawadu Bakilana, alipotembelea na kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya maji katika maeneo ya Nala, Zuzu, na Nzuguni jijini Dodoma.
Akiwa katika mradi wa maji wa Nzuguni, Ndugu Bakilana ameeleza kuridhishwa kwake na viwango vya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii inayozunguka maeneo hayo na Jiji la Dodoma kwa ujumla.
Ndugu Bakilana amebainisha kuwa, licha ya changamoto za upatikanaji wa maji zinazotokana na ongezeko kubwa la watu ukuaji na wa kasi wa jiji la Dodoma, jitihada zinazofanywa na DUWASA zimesaidia kufanikisha upatikanaji wa maji kwa asilimia 91 kwa Jiji la Dodoma.
"Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika sekta ya maji hapa Dodoma unaenda vizuri sana na kwa kasi ya kuridhisha. Hali ya upatikanaji wa maji kwa sasa imefikia asilimia 91 katika Jiji letu. Hili ni dhihirisho la kusudio la dhati la CCM na Serikali yake kuhakikisha tunamaliza kabisa kero ya maji, ambapo lengo letu kuu ni kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa maji ifikapo mwaka 2030," alisema Ndugu Bakilana.
Ziara hiyo ya ukaguzi ni sehemu ya mikakati ya CCM Mkoa wa Dodoma ya kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kulingana na ahadi za chama Tawala.
Kupitia ziara hiyo, CCM imetoa wito kwa DUWASA kuendelea kudumisha kasi hiyo na kuwataka wananchi kuilinda miradi hiyo ya maji ili iweze kudumu na kuleta tija iliyokusudiwa kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.